
Kwa ufupi
“Matukio ya kukojolewa kwa kitabu kitakatifu
(Quran), kuchomwa moto kwa baadhi ya makanisa na kuongezeka kwa vuguvugu
za kidini, ni baadhi ya mambo ambayo nayaona kuwa hayakushughulikiwa
ipasavyo na hili ni doa kubwa kwa utawala wa Rais Kikwete,” alisema
Profesa Lipumba.
WANASIASA wametoa tathmini ya utendaji wa Serikali ya Rais
Jakaya Kikwete kwa mwaka 2012, huku wakibainisha upungufu katika maeneo
kadhaa ambayo wameishauri iongeze nguvu kuyatekeleza mwaka huu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema pamoja
na Rais Kikwete kujisifu kwamba Serikali yake imefanikiwa mambo mengi,
kuna maeneo mengi ya msingi ambayo hayakufanikiwa.
Katika salamu zake za mwaka mpya Desemba 31, 2012,
Rais Kikwete alifafanua mambo mbalimbali ambayo Serikali yake
ilifanikiwa kuyatekeleza mwaka uliopita kwenye sekta za elimu, afya,
kilimo, nishati na gesi, miundombinu na barabara, huku akikiri pia
changamoto katika maeneo kadhaa.
“Mwaka tunaoumaliza leo ulikuwa wenye mambo mengi
mazuri na mafanikio makubwa, lakini ulikuwa na changamoto zake. Baadhi
zilikuwa ngumu na zipo zilizokuwa za kusikitisha na kuhuzunisha,”
alisema Rais Kikwete.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema
kwamba baadhi ya maeneo Rais aliyoshindwa kuyafanikisha ni utekelezaji
wa Kilimo Kwanza... “Nenda kamuulize mzazi wako, najua ni mkulima kule
kijijini.
Akuelezee kama anajua chochote kuhusu Kilimo
Kwanza. Wanayosema viongozi wa Serikali ni siasa tu hakuna mikakati ya
kiutendaji,” alisema Dk Slaa.
“Kutofanikiwa kwa Kilimo Kwanza kunatokana na
mikakati isiyo makini. Serikali iliagiza matrekta, lakini ikashindwa
kuyasimamia na hata kuwajengea uwezo wananchi katika kutekeleza mbinu za
mapinduzi hayo.”
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema
utendaji wa Serikali mwaka jana 2012 haukuwa wa kuridhisha, ingawa kuna
mwonekano wa mafanikio.
“Katika utendaji wake, hakuna alama yoyote
iliyoongezeka, ameendelea (Rais) kushikilia alama ileile kama ya miaka
ya nyuma. Haimaanishi kwamba amekwenda chini, hapana. Jambo la msingi ni
kwamba amekuwa siyo mwepesi kusimamia mambo yake ya msingi.”
Lipumba alitaja baadhi ya mambo aliyosema kuwa
yamemtia doa Rais katika utendaji wake mwaka 2012 kuwa ni polisi
kuwaandama wananchi na wakati mwingine kujitokeza kwa vifo
vilivyohusishwa na utendaji mbaya wa jeshi hilo.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vilitumbukia kwenye
kashfa ya matumizi mabaya ya madaraka ikiwamo kusababisha vifo vya raia,
jambo ambalo linakwenda kinyume na misingi ya utawala bora.
Tumeshuhudia matukio ya raia kuuliwa kule Morogoro
na tukio la kuuliwa kwa mwandishi wa habari mkoani Iringa. Jambo la
kushangaza ni kwamba pamoja na matukio hayo kukithiri na Jeshi la Polisi
kuwa na mikono yake, lakini hakuna hatua makini na za wazi
zilizochukuliwa dhidi ya wahusika,” alisema Profesa Lipumba.
Wanasiasa waichambua Serikali ya JK 2012
Reviewed by bongo qualities
on
2:59 AM
Rating: