
Kwa ufupi
“Ndugu zangu kabla ya leo kuja hapa, tulikuwa katika
kikao cha kutafuta muafaka wa jambo hilo, ambacho kiliongozwa na Katibu
Mkuu Kiongozi na Watendaji toka ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Serikali,
Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa na suala la malipo tumekubali serikali italipa”
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, hatimaye
jana limeidhinisha kuliachia eneo la Lakilaki lililopangwa kujengwa
mji wa mfano wa Arusha (Arusha Safari Town) na kukabidhi hati miliki ya
ardhi hiyo, kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa
ajili ya ujenzi wa majengo ya Taasisi za Umoja ya Mataifa na Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki.
Uamuzi huo ulifikiwa jana katika kikao cha dharura
cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, ambacho kilihudhuriwa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) Hawa Ghasia, baada ya
Serikali kukubali kulipa mkopo uliokopwa na halmashauri hiyo Benki ya
Biashara ya Afrika (CBA), kiasi cha Sh8.6 bilioni sambamba na kurejesha
gharama za mradi huo kiasi cha Sh788.2 milioni na faida ambayo
halmashauri hiyo ingepata kiasi cha Sh5.6 bilioni.
Akizungumza mara baada ya madiwani hao kupitisha
maombi ya kuchukuliwa eneo hilo, Waziri Ghasia aliwapongeza madiwani
hao kwa kukubali kuliachia eneo hilo na kueleza Serikali itarejesha
gharama zote za halmashauri hiyo.
“Lengo la serikali kutolewa eneo hili kwa Wizara
ya Mambo ya Nje ni kuwapa Umoja wa Mataifa na taasisi zake, ikiwepo pia
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ili waweze kujenga majengo yao kwa
manufaa ya taifa zima,” alisema Waziri Ghasia.
Hata hivyo baadhi ya madiwani walieleza kutilia
shaka uamuzi wa Serikali kuchukuwa ardhi hiyo na kutoa ahadi kwa mdomo
ya kulipa gharama zote, hatua ambayo ilimlazimu waziri huyo, kutoa
ufafanuzi wa malipo ya halmashauri hiyo.
“Ndugu zangu kabla ya leo kuja hapa, tulikuwa
katika kikao cha kutafuta muafaka wa jambo hilo, ambacho kiliongozwa na
Katibu Mkuu Kiongozi na Watendaji toka ofisi ya Mwanasheria mkuu wa
Serikali, Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa na suala la malipo tumekubali serikali
italipa”alisema Waziri Ghasia.
Waziri huyo pia alisema, Rais Jakaya Kikwete
alikuwa akifuatilia kupatikana kwa ardhi hiyo na ameiondoa hofu
halmashauri hiyo kupoteza fedha ambazo tayari wametumia na ambazo
wangepata kama wangetekeleza mradi huo.
“Jamani mimi ni mtu mzima siwezi kuja hapa kusema
ahadi ambazo hazipo, ninawahakikishia mtalipwa na mimi tayari niliandika
barua kuelezea jambo hili naomba muiamini Serikali yenu ahadi hii siyo
yangu ni ya Serikali” alisema Waziri Ghasia.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha,
Halfani Hida alisema mradi wa awali kama ungetekelezwa tayari walikuwa
wamepima jumla ya viwanja 348 ambavyo vingegawanywa kwa wananchi na
kuipatia halmashauri hiyo mapato ya Sh13.3 bilioni, pia viwanja vya
biashara vingeingiza mapato ya Sh1.7 bilioni huku maeneo ya huduma
yalitarajiwa kuingiza Sh332.6 milioni.
Baraza la Madiwani Arusha lasalimu amri kwa Serikali
Reviewed by bongo qualities
on
2:40 AM
Rating:
